Jumatano 22 Aprili 2026 - 15:36
Lazima tuzuie ardhi za Kiislamu kubadilishwa kuwa uwanja wa vita vinavyofuatana/ Yanayotokea leo si tu mgongano wa kijeshi

Hawza/ Yanayotokea leo si tu mgongano wa kijeshi; bali ni tukio ambalo linaweza kuathiri mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu na hata msingi wa kimaadili wa mahusiano baina ya mataifa. Ikiwa katika mfumo wa kimataifa itajengeka kanuni kwamba inawezekana kulishambulia taifa katikati ya mazungumzo, basi hakuna tena taifa huru litakaloketi meza mazungumzo kwa kujiamini.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah A‘rafi, Mkuu wa vyuo vya elimu ya dini vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika barua yake kwa wanazuoni wa ulimwengu wa Kiislamu ameandika: Wito wa barua hii, kabla ya yeyote, unalenga kwenu nyinyi wanazuoni na wanamageuzi wa umma wa Kiislamu; ili kwa kutetea misingi ya pamoja ya Kiislamu — heshima ya uhai wa mwanadamu, ubaya wa uchokozi, kushikamana na ahadi, na uhalisia wa mazungumzo — kuzuia kubadilishwa ardhi za Kiislamu kuwa uwanja wa vita vinavyofuatana.

Matini ya barua ni kama ifuatavyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Waheshimiwa wanazuoni na wanamageuzi wa ulimwengu wa Kiislamu

Amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake

«قال الله تعالی: إِنَّمَا یَخْشَی اللَّهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ»

Historia ya Uislamu inashuhudia kwamba katika nyakati ngumu zaidi, zenye giza zaidi na zenye migogoro mikubwa zaidi katika maisha ya umma wa Kiislamu, hakuna nguvu iliyoweza kama wanazuoni wa kweli wa dini kuelekeza njia ya jamii ya Waislamu kutoka katika mshangao na wasiwasi kuelekea kwenye mabadiliko, ukuaji na ustawi. Wanazuoni ambao kwa ujasiri, kwa kutafakari kwa kina Qur’ani, kwa ufahamu wa mwanadamu na zama zao, na kwa roho iliyojaa uwajibikaji mbele ya Mungu na viumbe Wake, katika kila ardhi na kila hali waliyokuwamo, wamekuwa kama bendera iliyoinuliwa wakionesha njia; kama taa yenye mwanga mkali wakimulika njia; na wakati mwingine kama jahazi la wokovu, wakiongoza waliopotea katika mawimbi ya dhoruba ya jamii kuelekea ufukwe wa amani.

Leo pia ulimwengu wa Kiislamu uko katika mojawapo ya vipindi vyake tata na vyenye misukosuko zaidi katika historia yake ya kisasa. Kwa upande mmoja, fursa za kipekee za kurejea katika heshima, uhuru na ustawi wa ustaarabu zimefunguliwa mbele ya umma wa Kiislamu, na kwa upande mwingine vitisho na migogoro mikubwa vimejificha vikinyemelea mwili huu mmoja. Katika hali hii nyeti, inaonekana hakuna jambo lenye uwezo kama uamsho, uoni wa mbali na ujasiri wa wanazuoni wa umma wa Kiislamu katika kuangaza njia ya baadaye na kuuongoza umma kuvuka milima migumu ya kipindi hiki.

Hatima ya ubinadamu, usalama na utulivu wa jamii, na kuwepo kwa mazingira huru na salama kwa ajili ya kukua kwa elimu, utamaduni na dini, daima vimekuwa katika kitovu cha uangalizi wa wanazuoni wa kweli wa dini. Katika mantiki ya Qur’ani Tukufu na katika mwenendo wa Mtume Mtukufu (saww) na viongozi wa uongofu, kiini cha Uislamu kimejengwa juu ya msingi wa amani, usalama na kuhifadhi heshima ya mwanadamu; amani ambayo si kutokana na udhaifu, bali kutoka katika msimamo wa hekima, uadilifu na uwajibikaji kwa hatima ya umma wa binadamu.

Uzoefu wa historia ya Uislamu pia unaonesha kwamba; kila mara wanazuoni wa dini walipokuwa na mshikamano na maingiliano yenye kujenga, mazingira ya ukuaji na maendeleo ya ulimwengu wa Kiislamu pamoja na kuundwa kwa mahusiano yenye afya kati ya mataifa yalikuwa rahisi zaidi. Kinyume chake, kila mara safu za wanazuoni zilipokumbwa na mgawanyiko na mielekeo myembamba ya kimadhehebu au ya kifirqa ilipotawala mtazamo mpana wa umma wa Kiislamu, mazingira ya fitna na migogoro mikubwa viliandaliwa; kiasi kwamba wakati mwingine wanazuoni, badala ya kutazamana katika upeo wa umma mmoja, walichambua hali ya wenzao kupitia mitazamo ya makundi madogo na bila kukusudia wakachangia katika kuimarisha mipasuko.

Historia ya Uislamu inathibitisha kwamba; wanazuoni wa madhehebu yote ya Kiislamu wamekuwa na nafasi isiyo na kifani katika kulinda mshikamano wa umma. Nafasi hii haijafungamana na dhehebu maalum wala eneo maalum la kijiografia; bali ina mizizi katika ukweli wa pamoja: mwelekeo wa kuelekea umoja na mshikamano chini ya mwanga wa imani kwa Mungu Mmoja na Mtume wa Mwisho.

Pamoja na hayo, katika historia kumekuwepo juhudi nyingi za kuyafanya mahusiano ya wanazuoni yaingizwe katika siasa na kuwavuta katika uwanja wa ushindani wa madaraka. Ingawa juhudi hizi wakati mwingine zimefanya hali ya umma wa Kiislamu kuwa tata, lakini katika nyakati nyeti za historia, ni wanazuoni hawa hawa walioweza kwa uoni wa mbali na hisia zao za uwajibikaji wa kihistoria kuzuia kuporomoka kukubwa.

Bila shaka, hatima ya jamii za Kiislamu inategemea zaidi namna wanazuoni wa Uislamu wanavyoshirikiana wao kwa wao na na jamii. Ikiwa ushirikiano huu utajengwa juu ya msingi wa hekima na mtazamo wa ustaarabu, upeo mpya wa matumaini na mshikamano utafunguka; na ikiwa — Mungu apishe mbali — kutokana na kutoelewana na uchochezi wa nje utakatika, basi njia ya kuingiliwa na migogoro mikubwa itafunguliwa.

Leo pia moja ya mikakati inayojulikana ya maadui wa ulimwengu wa Kiislamu ni kuwaweka wanazuoni wa Kiislamu katika mipaka myembamba ya kimadhehebu na kwa kukuza hisia za kifirqa, kudhoofisha roho ya umoja wa umma. Wanajua vyema kwamba ikiwa mwanazuoni Muislamu ataangalia masuala kwa upeo mpana wa ulimwengu wa Kiislamu, ataweza kutambua kwa usahihi maadui halisi wa ubinadamu na wa umma wa Kiislamu; na hasa hilo ndilo jambo ambalo hawataki litokee.

Huenda katikati ya moto wa vita na uharibifu uliosalia kutokana na milipuko — wakati miili laini ya wasichana wadogo wa shule huko Minab ikipasuliwa katika udongo na damu — kuzungumzia historia ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa mtazamo wa kwanza kukaonekana si jambo linalofaa; lakini ukweli ni kwamba kuelewa matukio mengi ya leo bila kuzingatia asili ya mapinduzi hayo haiwezekani.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kwa ushuhuda wa baadhi ya wanafikra wakubwa wa kijamii Mashariki na Magharibi, hayakuwa tu tukio la kisiasa au lililofungamana na dhehebu maalum; bali yalikuwa tukio la kibinadamu–Kiislamu lenye upeo unaovuka mipaka ya kabila na firqa. Mapinduzi haya yalilenga kuonesha tena uwezekano wa kuunganisha dini, heshima, uhuru na maendeleo katika ulimwengu wa kisasa na kuwakumbusha Waislamu kwamba; inawezekana kusimama dhidi ya mifumo ya ubeberu huku wakishikamana na utambulisho wa kidini na heshima ya kibinadamu.

Katika zaidi ya miongo minne iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijaanzisha vita wala haijaingia kwa hiari yake katika mgongano wa kijeshi na nchi yoyote; ingawa vita vingi zimeilazimishwa. Jambo muhimu hapa ni mantiki inayotawala sera ya Iran: juhudi endelevu za kuepuka vita na kutoa kipaumbele kwa mazungumzo na suluhisho za kidiplomasia katika kutatua migogoro.

Katika miaka ya mwanzo baada ya mapinduzi, vita vya miaka minane vililazimishwa dhidi ya Iran; vita vilivyoanza katika siku ngumu zaidi za kuimarika kwa mfumo mpya wa Jamhuri ya Kiislamu. Katika kipindi hicho, baadhi ya nchi za eneo na nguvu za dunia zilisimama upande wa mpinzani kwa msaada wa kifedha, kijeshi na kisiasa, na matokeo yake yakawa hasara kubwa za kibinadamu na mali kwa mataifa mawili ya Kiislamu.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa vita, Iran badala ya kulipa kisasi au kudai fidia kubwa, kwa matumaini ya busara na uelewa wa pamoja wa hali ya ulimwengu wa Kiislamu, iliacha madai mengi yake na kuchukua njia ya uvumilivu na ustahimilivu.

Licha ya mtazamo huu, katika miaka iliyofuata juhudi kubwa zilifanywa kuharibu taswira ya Iran katika fikra za umma wa ulimwengu wa Kiislamu. Lugha ya takfiri na upotoshaji ikaenea, na katika baadhi ya matukio ushirikiano na utawala wa Kizayuni na Marekani ukaundwa kwa ajili ya kusukuma mbele malengo yao katika eneo.

Katika mwelekeo huu, sehemu za eneo zikawa uwanja wa aina fulani ya muafaka wa kimkakati na utawala wa Kizayuni, na mipaka ya kusini ya Iran polepole ikageuka kuwa sehemu ya uwepo mkubwa wa kambi za kijeshi za Marekani.

Hatimaye katika miezi ya hivi karibuni, hatua mpya ya mchakato huu ilitokea. Takribani mwezi mmoja sasa, vita vilivyolazimishwa na uchokozi wa wazi kutoka Marekani na utawala wa Israel kwa msaada wa baadhi ya serikali nyingine dhidi ya taifa na serikali ya Iran vimeanza. Katika mashambulizi haya, maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia waliuawa kishahidi, na mbali na hao, baadhi ya makamanda, viongozi na juu yao kiongozi mkubwa wa kidini na Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mtukufu Ayatullah Khamenei, pia waliuawa kishahidi.

Katika mashambulizi haya, zaidi ya nyumba elfu sitini na mamia ya vituo vya kisayansi, tiba na kijamii, makumi ya viwanda na sehemu za miundombinu ya nishati, viwanda na mawasiliano viliharibiwa au kuangamizwa. Kiasi hiki cha uharibifu hakikuwa tu operesheni ndogo ya kijeshi; bali ni mfano wa wazi wa vita ambavyo athari zake za kibinadamu na kiustaarabu zinagusa eneo zima.

Kinachofanya tukio hili kuwa tata zaidi ni kwamba shambulio hili lilifanyika wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwa kwa mara ya pili katika njia ya mazungumzo na Marekani. Hivyo, katikati ya mchakato wa mazungumzo, meza ya mazungumzo ilivunjwa kwa makombora na mabomu; hatua ambayo kwa hakika hailengi tu nchi moja, bali inalenga pia msingi wa mazungumzo na uaminifu katika mahusiano ya kimataifa.

Mbele ya tukio hili, jambo la kusikitisha ni kwamba; baadhi ya serikali, licha ya kudai ujirani na udugu wa Kiislamu, zilitoa ardhi, anga na maji yao ya kieneo kwa vikosi vilivyotekeleza shambulio hili. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kwamba inazichukulia nchi za eneo kuwa ndugu na majirani wake, na majibu yake yataelekezwa tu kwenye kambi ambazo kutoka humo mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran yanafanywa; majibu ambayo yanafafanuliwa ndani ya haki ya kujilinda kisheria.

Yanayotokea leo si tu mgongano wa kijeshi; bali ni tukio ambalo linaweza kuathiri mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu na hata msingi wa kimaadili wa mahusiano baina ya mataifa. Ikiwa katika mfumo wa kimataifa itajengeka kanuni kwamba inawezekana kulishambulia taifa katikati ya mazungumzo, basi hakuna tena taifa huru litakaloketi mezani pa mazungumzo kwa kujiamini.

Katika hali kama hii, nafasi ya wanazuoni wa dini katika ulimwengu wa Kiislamu inakuwa muhimu mara dufu. Wao katika historia wamekuwa walinzi wa dhamiri ya kimaadili ya umma, na katika nyakati nyeti kwa maneno yaliyo wazi wameweza kubadilisha mwelekeo wa migogoro mingi.

Leo pia swali la msingi ni hili: je, ulimwengu wa Kiislamu unaweza kubaki kimya mbele ya mienendo inayodhoofisha uhuru wa mataifa ya Kiislamu? Je, inawezekana kukaa kimya mbele ya kubadilishwa kwa ardhi za Kiislamu kuwa uwanja wa mashindano ya nguvu za dunia?

Bila shaka Qur’ani Tukufu inawalingana Waislamu kwenye heshima, umoja na kuepuka udhaifu: «وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الأَعْلَوْنَ إِن کُنتُم مُّؤْمِنِینَ». Kutimia kwa ujumbe huu wa Qur’ani kunahitaji zaidi ya wakati mwingine wowote uono wa mbali, ujasiri na mshikamano wa wanazuoni wa Kiislamu.

Kwa hiyo, wito wa barua hii, kabla ya yote, unalenga kwenu nyinyi wanazuoni na wanamageuzi wa umma wa Kiislamu; ili kwa kutetea misingi ya pamoja ya Kiislamu — heshima ya uhai wa mwanadamu, uchokozi, kushikamana na ahadi, na uhalisia wa mazungumzo — kuzuia kubadilishwa kwa ardhi za Kiislamu kuwa uwanja wa vita vinavyofuatana.

Bila shaka historia itahukumu mwenendo na misimamo yetu sote katika siku hizi ngumu. Vizazi wajao watauliza kwamba; wanazuoni wa dini walifanya nini katika kipindi hiki nyeti: je, walijishughulisha na tofauti ndogo ndogo au walijitokeza kulinda heshima ya umma wa Kiislamu?

Inatarajiwa kwamba sauti ya hekima na mshikamano wa wanazuoni wa Uislamu itasikika tena na kufungua njia ambayo ndani yake mazungumzo yatachukua nafasi ya vita na mshikamano kuchukua nafasi ya mgawanyiko.

Mwisho, kwa matumaini kwamba sauti ya uwajibikaji wa wanazuoni wa Uislamu itafungua upeo mpya mbele ya umma wa Kiislamu, tunanyoosha mkono wa udugu na mazungumzo kwenu nyote na tunatumai kwamba kwa ushirikiano wa mawazo na moyo mmoja, hatua itachukuliwa katika kupunguza mateso ya wanadamu, kulinda usalama wa mataifa na kuimarisha heshima ya ulimwengu wa Kiislamu.

Na amani iwe juu yenu na rehema za Mwenyezi Mungu na baraka zake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha